Mjadala unaondelea Kenya kuhusu kesi za uhalifu za watu maarufu umefunua kiasi kidogo tunachojua kuhusu jinsi kesi za uhalifu zinavyosikizwa. Hakuna wakati bora kama sasa kwa umma kujifunza mchakato wa kushtaki mtu kwa uhalifu.
Maarifa haya ni muhimu kwani yanaweza kusaidia walalamikaji, washukiwa, na wale waliohusika nao kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha kushindwa kwa haki.
Hatua za kushtaki mtu kwa uhalifu kawaida hufuata hatua muhimu hizi nchini Kenya:
kuwasilisha malalamishi
Hatua hii ya awali hufanyika katika kituo cha polisi, ambapo mlalamikaji anawasilisha malalamiko, yanayosajiliwa kwa usahihi katika kitabu cha tukio. Mlalamikaji kisha hupokea nambari ya kumbukumbu ambayo ni muhimu kwa ajili ya ufuatiliaji wakati wa uchunguzi.
Uchunguzi:
Polisi au mamlaka husika ya utekelezaji wa sheria inafanya uchunguzi wa uhalifu uliodaiwa. Hii inajumuisha kukusanya ushahidi, kufanya mahojiano na mashahidi, na kukusanya habari muhimu. Kwa kuongezea, taarifa kutoka kwa mlalamikaji na mashahidi wao husika zinaweza kudhibitishwa, hatua ambayo itasababisha kuandikwa kwa mashtaka.
Kukamatwa:
Kama uchunguzi unatoa ushahidi wa kutosha, mtuhumiwa anaweza kukamatwa. Kukamatwa lazima kufanyike kwa kufuata taratibu za kisheria, na haki za mtuhumiwa zinapaswa kuheshimiwa.
Dhamana:Baada ya kukamatwa, mtuhumiwa anaweza kuachiliwa kwa dhamana kutegemea ukali wa kosa. Kwa makosa madogo, mtuhumiwa anaweza kutolewa tiketi na maelekezo ya kufika mahakamani.
Kushtakiwa:
Baada ya kukamatwa, mtuhumiwa anashtakiwa rasmi na kosa lililodaiwa. Hii inajumuisha kurekodi maelezo ya kosa, sheria iliyokiukwa, na pande zinazohusika kwenye karatasi ya mashtaka. Kesi kisha hupelekwa kwa mwendesha mashtaka wa serikali kwa tathmini ya ushahidi wa kutosha.
Kufikishwa Mahakamani na Kutolewa Kauli ya Mashtaka
Washukiwa wanaletwa mbele ya Mahakama na kusomewa mashtaka. Wanatakiwa kujibu mashtaka hayo kwa kukiri au kuto kukiri. Kukiri kunapelekea kuhukumiwa mara moja ikiwa kesi ni kali au kuachiwa huru kwa makosa yasiyo na uzito. Kutokukiri kutaendeleza kesi hiyo kusikizwa mahakamani.
Kusikilizwa kwa Dhamana
Baada ya kusomewa mashtaka, washukiwa wanaweza kuombewa dhamana ili waachiliwe wakiwa nje ya jela hadi kesi yao itakaposikilizwa. Mambo kama hatari ya kukimbia na ukali wa kosa huzingatiwa katika kusikiliza hii. Ushahidi kutoka pande zote mbili, upande wa mashtaka na utetezi, hutolewa kwa kuzingatiwa na mahakama. Kukubaliwa kwa dhamana kunahusisha malipo ya fedha hadi kufika kwa kesi za baadaye; kukataliwa kunapelekea kuzuiliwa, na kesi kutajwa kila baada ya wiki mbili.
Kesi Mahakamani:
Kesi hufunguliwa, ambapo upande wa mashtaka na utetezi huleta ushahidi wao mbele ya afisa wa mahakama. Upande wa mashtaka huanza na taarifa za kuanza kesi, kufuatiwa na kutoa sheria, ushahidi, na mashahidi. Upande wa utetezi huchukua nafasi yake kwa kutoa ushahidi wao, ushahidi wa sheria husika, mashahidi, na ushahidi mwingine. Kila upande una nafasi ya kuhoji mashahidi wa upande mwingine. Baada ya hapo, pande zote mbili hutoa kauli za mwisho kabla ya jaji kufanya uamuzi.
Hukumu:
Baada ya kusikiliza ushahidi wote na hoja, jaji hutangaza uamuzi wa hatia au kutokuwa na hatia. Ikiwa mshitakiwa amepatikana na hatia, mahakama huendelea na kutoa adhabu.
Kutoa Adhabu:
Baada ya kuhukumiwa, jaji anatoa adhabu kwa kuzingatia mwongozo maalum wa adhabu kwa kosa husika.
Mazingira ya Kupunguza Adhabu:
Upande wa utetezi unaweza kuwasilisha mazingira ya kupunguza adhabu, kama vile kuwa ni kosa la kwanza, umri mkubwa, au kuwa mlezi wa familia. Mara jaji anapotoa adhabu, kesi hufungwa. Kila upande una haki ya kukata rufaa kuzingatia sheria zilizoko.
Rufaa
Wote upande wa mashtaka na utetezi wana haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi au adhabu ikiwa wanaamini kuna makosa katika mchakato wa kesi au ikiwa ushahidi mpya unaibuka.